Gwaride kubwa kabisa la kijeshi Moscow
Rais Vladimir Putin wa Urusi Jumamosi (09.05.2015) asimamia gwaride
kubwa kabisa la kijeshi kuadhimisha miaka sabini ya ushindi dhidi ya
Wanazi wa Ujerumani na kupuuza bebeduo la mataifa ya magharibi kususia
sherehe hizo
Makombora ya kutoka ardhini kwenda angani yakionyeshwa katika gwaride
la kijeshi kusheherekea Siku ya Ushindi Moscow. (09.05.2015)
Kwa kile kinachoonekana kama kuadhibiwa kutokana na hatua yake ya
kuingilia mambo ya ndani ya Ukraine,viongozi wa mataifa ya magharibi
washirika wa Urusi katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia wamezisusia
sherehe hizo za Mei 9 na kumuachilia Putin aziadhimishe kwa
kushindikizwa na viongozi wa China,Cuba na viongozi wengine wenye
uhusiano mzuri na Urusi.Akiwahutubia maelfu ya wageni kutoka nje na wanajeshi wakongwe, Putin amepuuza kususiwa huko na kuzishukuru Uingereza,Ufaransa na Marekani kwa mchango wao katika kuushinda utawala wa Wanazi wa Ujerumani.
Putin amesema
"baba zetu na babu zetu walikabiliwa na mateso yasiovumilika,hasara na kujinyima."Mbali ya kuzishukuru Uingereza, Ufaransa na Marekani kwa mchango wao katika ushindi huo pia amewashukuru wale waliopambana na Wanazi katika nchi nyengine ikiwemo Ujerumani.
Kijembe kwa Marekani
Katika kile kinachoonekana kama kijembe kwa Marekani Putin ameshutumu jaribio la kuanzisha mfumo wa dunia utakaodhibitiwa na taifa moja yaani Marekani na kusisitiza haja ya kuanzisha mfumo wa usawa wa usalama kwa mataifa yote.Hata hivyo hakutowa kauli za majigambo ya shari na hakuutaja mzozo wa Ukraine.
Zaidi ya wanajeshi 16,000 wakiwemo wale wa China, Mongolia,Serbia na majimbo kadhaa ya Muungano wa zamani wa Kisovieti walishiriki katika gwaride hilo.Putin alikuwa ameketi pembezoni kwa Rais Xi Jinping wa China wakati gwaride hilo lilipokuwa likipita katika uwanja maarufu wa Kremlin Ikulu ya Urusi mjini Moscow.
Zana za kisasa kabisa za kijeshi vikiwemo vifaru vya kizazi kijacho chapa T-14 na mifumo ya kufyetulia makobora ya nyuklia ilirindima kwenye uwanja huo wakati wa sherehe hizo kubwa kabisa za ushindi wa vita kuwahi kushuhudiwa kwa miongo kadhaa.Gwaride la mwaka huu pia lilishuhudia zaidi ya ndege za kivita mia moja zikiwemo zile za makombora ya nyuklia zikivinjari kwa shani katika anga ya Moscow.
Ari ya taifa
Muungano wa Kisovieti ulipoteza maisha ya wanajeshi na raia wanaokadiriwa kufikia milioni 27 katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia kuliko nchi nyengine yoyote ile na ushindi wa Jeshi Jekundu la nchi hiyo unaendelea kubakia kuwa chanzo kikuu cha ari ya taifa hilo.Siku hii ya Ushindi huwaunganisha wananchi wote wa Urusi bila ya kijali ufuasi wao wa kisiasa na umma mkubwa umemiminika katikati ya mji mkuu wa Moscow.
Sherehe za gwaride hilo katika Ikulu ya Urusi Kremlin zimetiwa kiwingu na mzozo wa Ukraine ambapo mataifa ya magharibi yameiwekea vikwazo Urusi kutokana na hatua ya nchi hiyo kulinyakuwa jimbo la Ukraine la Crimea na kuwaunga mkono waasi wanaotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine.
Rais Barack Obama wa Marekani amezipa kisogo sherehe hizo kama walivyofanya viongozi wa washirika wa Urusi wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia yaani Uingereza na Ufaransa.
Kiwingu cha mzozo wa Ukraine
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani pia amekwepa kuhudhuria sherehe hizo lakini atakwenda Moscow Jumapili kuweka shada la mauwa katika kaburi la askari asiejulikana na pia kukutana na Rais Putin.
Mbali na Rais Jinping wa China viongozi wengine wakuu mashuhuri waliohudhuriua sherehe hizo ni pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon na Rais wa India Pranab Mukherjee.Sherehe hizo pia zimehudhuriwa na Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri,Raul Castro wa Cuba, Nicolas Maduro wa Venezuela, Robert Mugabe wa Zimbabwe na Jacob Zuma wa Afrika Kusini.
Urusi imesema haikumualika Rais Petro Poroshenko wa Ukraine kuhudhuria sherehe hizo.Serikali ya Urusi pia imezitumia simulizi za Vita Vikuu vya Pili vya Dunia kushawishi kuungwa mkono kwa agenda yake ya kisiasa kwa mfano kwa kuipakazia serikali ya Ukraine kuwa ni wafuasi wa Wanazi.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP
No comments:
Post a Comment